dc.description.abstract |
Mawasiliano yameimarika sana katika karne ya ishirini na moja kufuatia uvumbuzi wa
teknolojia ya habari na matumizi ya intaneti. Kuimarika kwa hali ya kutangamana kwa
watu kwenye mitandao kumeongeza visa vya uhalifu. Mawasiliano ya mitandaoni
yamesababisha kuwepo kwa diskosi nyingi za mitandaoni ambazo ni tofauti na diskosi
za maandishi na za mazungumzo ya moja kwa moja. Uhalifu wa mitandaoni ni uovu
ambao umekuwepo kutoka wakati ambao uvumbuzi wa intaneti ulipotokea. Wahalifu
wa mitandaoni hutumia baruapepe, Instagram, Twitter, Facebook, To-go WhatsApp na
njia nyingine nyingi za mitandao kuwadanganya na kuwaibia watu hela. Lugha
hutumika katika mitandao hii kuwashawishi watumiaji ili kuingia katika mitego yao
miovu. Wahalifu hutuma jumbe za ushindi wa pesa, ugawaji urithi, jumbe za
kibiashara, udukizi, uduhushi na utoaji wa pesa na ulaghai wa ushindi katika michezo
ya kamari. Utafiti huu ulichunguza aina mbalimbali za uhalifu katika mitandao ya
Facebook na baruapepe, kuchanganua mikakati ya ushawishi inayotumiwa na wahalifu
na kuhakiki mbinu za lugha katika jumbe za kihalifu katika mitandao hii miwili.
Nadharia ya Uchanganuzi wa Mawasiliano ya Kiupatanishi ya Kitarakilishi ya Herring
pamoja na nadharia ya Ushawishi iliyoasisiwa na Aristotle kisha kuendelezwa na
Hovland na Cialdini zilitumika. Utafiti huu ulifanyika maktabani huku ukihusisha
ukusanyaji wa data kwa njia ya kupakua jumbe pamoja na picha katika mitandao ya
Facebook na baruapepe. Mbinu ya kiuthamano ilitumiwa katika uchanganuzi wa data.
Muundo wa utafiti ulikuwa wa kimaelezo kwa kutoa ufafanuzi wa mambo yote kwa
kina katika kila hatua. Sampuli ya utafiti iliteuliwa na mtafiti kimakusudi kwa kutumia
jumbe na picha mia moja ambazo baadaye zilichujwa hadi arubaini na saba mintaarafu
ya madhumuni ya utafiti. Data iliyokusanywa ilionyesha kuwa mikakati ya ushawishi
kama vile imani na maadili, utoaji wa hoja zenye mantiki na hisia hutumiwa sana
kushawishi watumiaji wa mitandao hii hadi kufikia kiwango cha kuwatapeli watumiaji.
Vilevile, ilibainika kuwa wahalifu wa mitandaoni hutumia mbinu nyingiza lugha kama
vile takriri, mdokezo, mbinu rejeshi, nidaa, imoji, simulizi, maswali ya balagha na
nyinginezo ikiwa ni njia moja ya kufaulisha mazungumzo yao na kushawishi watumiaji
wa mitandao. Utafiti pia ulibainisha kuwepo kwa aina mbalimbali za uhalifu kwenye
mitandao hii kama vile utapeli, uumbuaji, unyanyasaji wa kimapenzi, vitisho, ubaguzi
na propaganda za kiuchochezi. Utafiti huu utawafaa wasomi na watafiti wa lugha kwa
sababu, utawezesha watafiti wengine kuwa na ari ya kuchambua diskosi na kauli tofauti
tofauti kama zinavyotumiwa na watu katika mitandao na kuweza kupambanua maana
kwenye muktadha. Zaidi ni kuwa matokeo yake yataongeza maarifa kwa watafiti kwa
kuchambua namna nadharia ya Mawasiliano ya Kiupatanishi ya Kitarakilishi na ya
ushawishi zinaweza kutumiwa kubainisha mitindo mbalimbali ya matumizi ya lugha
na mikakati ya mawasiliano ambayo huonyesha dalili za uhalifu wa mitandaoni na jinsi
ufahamu huu unaweza kutumiwa kama mikakati ya kujizuia na kupunguza uhalifu wa
mitandaoni. |
en_US |