Abstract:
Fasihi ya watoto inaweza kufasiliwa kama kazi ya sanaa inayotungwa ikilenga watoto kama
hadhira kuu. Fasihi hii hutungwa na kuhakikiwa kwa misingi ya kanoni ambazo ni vigezo
vya kupimia ubora wa fasihi hii. Vigezo hivi vinatokana ama na kazi ambazo zilifana sana
kiasi cha kuigwa au na sifa za fasihi ya watoto zilizotolewa na wataalamu na ambazo
imekuwa kama ni mwiko kuzikiuka. Hata hivyo, kumetokea waandishi wa hadithi za watoto
wanaotunga kazi zilizokiuka kanoni ya fasihi hii kimaudhui na kifani. Maudhui ambayo
yalichukuliwa kuwa yanafaa kushughulikiwa tu katika fasihi ya watu wazima, yanaanza
kujipenyeza katika hadithi za watoto huku baadhi ya sifa za fani pia zikikiukwa. Kuna haja
basi ya kuchunguza ni vipi ukiushi huu unavyojitokeza na kudhibitiwa ili hadithi
ifungamane na tajriba ya watoto wanaolengwa. Madhumuni halisi ya utafiti huu yalikuwa
kuchunguza ukiushi wa kanoni ya maudhui katika hadithi teule za watoto za John Kobia na
Wadi Wamitila; kuchanganua ukiushi wa kanoni ya fani katika hadithi teule za watoto za
John Kobia na Wadi Wamitila na kutathmini mikakati ambayo waandishi wa hadithi teule
wanatumia kudhibiti ukiushi wa kanoni. Utafiti huu ulitumia nadharia ya udenguzi ya
Derrida (1976) na nadharia ya umitindo ya Leech (1969). Nadharia ya udenguzi ilitumiwa
kutathminia ukiushi wa maudhui na fani. Utafiti huu uliongozwa na mihimili mikuu mitatu
ya nadharia hii. Nadharia ya umitindo ilitumiwa kuchunguzia ukiushi wa fani na pia
kutathminia mikakati ya kiubunifu aliyotumia mwandishi kudhibiti ukiushi. Mihimili
mikuu mitatu ya nadharia ya umitindo iliongoza utafiti huu. Huu ulikuwa utafiti wa
kimaelezo. Hadithi za watoto za waandishi hawa ziliteuliwa kimakusudi kwa kutumia
sampuli lengwa kutokana na upekee wa kimaudhui na kifani uliodhihirisha ukiushi.
Ilibainika wameandika hadithi kadhaa zenye ukiushi. Hadithi zilizoteuliwa zilisomwa
kukusanya data kuhusu ukiushi wa kanoni kwa kujibu maswali ya utafiti. Data iliyopatikana
kuhusu ukiushi wa kanoni katika kila hadithi ilichanganuliwa. Mwisho, matokeo na
mapendekezo ya utafiti yaliwasilishwa kimaelezo. Matokeo yalibainisha kuwa hadithi
zilizochunguzwa zilikiuka kanoni ya fasihi ya watoto kimaudhui na kifani lakini kwa njia
iliyodhibitiwa. Utafiti huu unatarajiwa kuwa muhimu kwa wasomi na waandishi wa fasihi
ya watoto. Unaongeza maarifa katika uhakiki wa hadithi za watoto kwa kuangazia mielekeo
ya kimaudhui na kifani inayokiuka kanoni.