Abstract:
Nyimbo kama zilivyo tanzu zingine za fasihi simulizi huhusisha matumizi ya mitindo
changamano katika kuwasilisha ujumbe wa kisiasa. Utafiti huu ulidhamiria kufanya
uchanganuzi wa mitindo ya nyimbo za kisiasa zilizoimbwa na wasanii watatu kutoka
Kaunti ya Murang’a: Joseph Kamaru, Kamande wa Kioi na John De’Mathew.
Ulilenga kutambulisha, kuainisha na kuchanganua vipengele vya kimtindo
vinavyotumiwa na wanamuziki hao na athari zake kwa wakaazi wa Kaunti ya
Murang’a. Pia, dhima inayotekelezwa na nyimbo za kisiasa katika kaunti hii
ilichunguzwa. Utafiti umelenga kuonyesha iwapo kuna aina mahususi ya mitindo
inayotumiwa na wanamuziki hawa. Aidha, utafiti huu umejikita katika kuweka wazi
iwapo nyimbo hizi huathiri maamuzi ya wanajamii wa Kaunti hii. Utafiti huu
umeegemea kwenye mihimili ya nadharia mbili: nadharia ya uhalisia na ya mtindo.
Uteuzi wa sampuli ulikuwa wa kimaksudi. Data ya utafiti huu ilikusanywa kwa
kusikiliza kanda za nyimbo za wasanii hawa na kuziainisha katika makundi mawili:
za kisiasa na zisizo za kisiasa. Mtafiti ameteua sampuli ya kimaksudi ya nyimbo kumi
na tano (15) za kisiasa- nyimbo tano (5) kutoka kila msanii kwa lengo la kuchanganua
vipengele vya kimtindo katika kila wimbo wa kisiasa. Wawakilishi Kaunti kumi na
sita (16) kutoka kaunti hii waliteuliwa kimaksudi na kuhojiwa ili kupata maoni yao
kuhusu maudhui katika nyimbo za kisiasa za wasanii Joseph Kamaru, Kamande wa
Kioi na John De’Mathew na athari yake kwa hadhira. Mahojiano hayo yaliongozwa
na ratiba ya mahojiano. Mtafiti alinasa kauli zao kwa tepurekoda na kuzitumia zikiwa
data ya utafiti huu. Maoni yao yalichanganuliwa ili kubainisha athari za nyimbo za
kisiasa za wasanii husika kwa wakaazi wa kaunti ya Murang’a. Uchanganuzi wa data
umefanywa kwa njia ya kithamano elezi. Matokeo ya utafiti huu yamedhihirisha
kwamba wasanii Joseph Kamaru na John De’Mathew hutumia jazanda, methali,
taswira, uhuishi na hurafa katika nyimbo zao za kisiasa katika kuwasilisha ujumbe wa
kisiasa. Utafiti huu umebainisha kuwa mitindo hiyo hutumiwa na wasanii kuwapigia
upatu wanasiasa, kuihamasisha, kuizindua na kuchochea hadhira yao katika kufanya
maamuzi ya kisiasa. Matokeo utafiti huu yatakuwa na manufaa kwa wasomi wa
Fasihi Simulizi kuhusiana na dhima ya fasihi katika jamii na vile vile kuhusiana na
taaluma ya Elimu – Mtindo.