Abstract:
Miviga za jandoni ni mojawapo ya tanzu za fasihi simulizi. Utanzu huu hutumiwa
kupitisha mafunzo kuhusu masuala ya ngono kwa wavulana wakiwa jandoni. Mafunzo
yanayohusu tendo la ndoa katika jamii yoyote huwa nyeti. Hata hivyo, hayazungumzwi
hadharani. Yanapojitokeza katika kauli za wanajamii, huwasilishwa kwa mikakati
mahususi ya kujaribu kuuficha uwazi huo. Ingawa wataalamu mbalimbali
wamechunguza diskosi za tendo la ndoa katika nyanja tofauti tofauti, uchanganuzi wa
diskosi za tendo la ndoa katika muktadha wa jandoni haujafanyiwa utafiti wa kina.
Utafiti huu hivyo basi, ulidhamiria kuchanganua diskosi za tendo la ndoa
zinavyojitokeza katika mafunzo ya jandoni katika jamii ya Wakipsigis. Malengo ya
utafiti yalikuwa kuchanganua mada za diskosi za tendo la ndoa na kutathmini mikakati
inayotumiwa katika mafunzo ya diskosi za tendo la ndoa katika shughuli za jando.
Utafiti huu ulielekezwa na Nadharia ya Diskosi hasa kwa Mkabala wa Historia.
Mihimili ya nadharia hii ni mikakati ya; urejelezi, uarifishaji, ubishi, mikabala,
kuongeza na kufifisha makali ya usemi. Asilimia kubwa ya utafiti huu ilikuwa ya
nyanjani, kwa ajili ya kukusanya data ya kimsingi. Aidha, mtafiti alihusisha utafiti wa
maktabani ili kupata michango ya wataalamu wa awali kuhusu suala hili. Data
ilikusanywa kwa njia ya mahojiano, kurekodi, picha na majadiliano. Jamii ya
Wakipsigis ndio ilikuwa kundi lengwa la utafiti huu na mafunzo yanayohusu suala la
tendo la ndoa jandoni yalilengwa. Data ya utafiti huu iliwasilishwa na kuchanganuliwa
kwa kutumia mbinu ya kimaelezo ili kudadavua matokeo ya utafiti. Utafiti huu
ulifanyika katika eneo la Bomet wanakoishi asilimia kubwa ya Wakipsigis. Ngariba
watatu waliteuliwa kutoka maeneo matatu makuu ambayo ni Kaunti ndogo za
Chepalungu, Bomet Mashariki na Sotik. Maeneo haya yaliteuliwa kwa kuwa yana
utamaduni asilia ambao haujaathiriwa na tamaduni za kigeni na usasa. Sampuli ya
utafiti huu ilihusisha kuteua watahiriwa wawili kutoka mfumo wa rika saba
inayopatikana kwa jamii hiyo ili kupata data ya kutegemewa. Matokeo ya utafiti
yameonyesha kwamba mada zinazozungumziwa ni; idhini ya kushiriki ngono, jinsi ya
kushiriki tendo la ngono, washiriki katika tendo la ngono, unyeti na maadili katika
tendo la ndoa. Baadhi ya mikakati inayotumiwa kupitisha mada hizi ni kama vile;
jazanda, taashira, tasfida, sitiari, nyimbo na istihizai. Utafiti huu ulinuia kuongeza
maarifa kwa wasomi, wahakiki na watafiti wa masuala ya uchanganuzi usemi. Matokeo
ya utafiti huu yatafaa wataalamu wa lugha, wachanganuzi wa diskosi na utachangia
kuelewa suala la diskosi katika muktadha wa jinsia. Aidha, utafiti huu utawaauni
washikadau wote wanaohusika katika kubuni sera zinazohusiana na jinsia..