Abstract:
Tangu maajilio ya vyama vingi vya kisiasa nchini Kenya lugha imekuwa ikitumiwa kama zana
ya kisiasa na kijamii katika kukuza ushindani na kukolezea mikakati ya usemi wa kikabila
ambao hunuiwa kutoa nafasi kwa mwanajamii kuyasimbua masuala fulani ya kijamii akilenga
faida imrudie yeye. Kutokana na mabadiliko kadhaa ya kisheria ambayo yalitokea nchini
Kenya baada ya uchaguzi wa 2007, haikuwa dhahiri ikiwa wanasiasa wangeusitiri usemi wao,
kwa kuhofia kufunguliwa mashtaka endapo ingebainika kuwa usemi wao ungekuza chuki
baina ya jamii mbalimbali nchini. Utafiti huu ulilinganua usemi wa wanasiasa miezi mitano
kabla ya chaguzi za mwaka wa 2007 na 2013. Malengo ya utafiti huu yalikuwa kuzichunguza
mada tofauti za usemi katika kampeni za urais nchini Kenya katika kipindi kilichokuwa chini
ya utafiti huu. Utafiti huu vilevile ulijadili mikakati tofauti tofauti iliyotumiwa na wanasiasa
katika kampeni za urais nchini Kenya; na kutathmini athari za usemi wa wanasiasa katika
kampeni hizo. Nadharia ya Uchanganuzi Hakiki wa Usemi (UHU): Usemi – Mkabala wa
Kihistoria (UMK) ilimwongoza mtafiti, ambapo mbinu ya maelezo ndiyo iliyotumiwa
kuichanganulia data. Wanasiasa waliolengwa walikuwa Raila Odinga, Uhuru Kenyatta na
William Ruto. Data ilikusanywa kwa njia ya kimakusudi (usampulishaji wa matukio
kiuhakiki) kutoka kwenye magazeti ya The Daily Nation na The Standard ambamo nukuu za
usemi wa wanasiasa hao za miezi mitano kabla ya chaguzi za mwaka 2007 na 2013
zilichanganuliwa. Mada za Usemi katika kampeni zilikuwa msingi wa uchanganuzi wa data
husika. Ilibainika kuwa uteuzi wa mada za usemi huongozwa na masuala nyeti ya kihistoria
katika jamii kama vile ardhi na masuala mengine ibuka. Aidha, ilibainika kuwa wanasiasa
huiteua mikakati mbalimbali ambayo malengo yake huwa ni kuishawishi jamii; isitoshe,
imedhihirika kwamba usemi huo wa kisiasa ulikuwa na athari kadhaa; kama vile, kujikariri
kwa masuala ya kihistoria, kuzalika kwa miungano ya kikabila, kuibuka kwa usemi wa
kitabaka, kuibuka kwa usemi wa kidini na kuchipuka kwa usemi wa kuumbuana miongoni
mwa matukio mengine mengi. Utafiti huu umeonyesha kuwa lugha ni kiashiria cha masuala ya
jamii na hivyo hali za kisiasa, hivyo basi, lugha inaweza kuonekana kama nguvu ya
kuendeshea mabadiliko ya kisiasa na kijamii. Inatarajiwa kwamba utafiti huu ni mchango
katika kuukuza uwanja wa uchanganuzi wa usemi wa kisiasa hasa ulinganuzi wa usemi wa
kisiasa. Mwisho, inatarajiwa kuwa matokeo yatachangia katika kuyaelekeza mashirika
mbalimbali ambayo yamepewa majukumu kuhakikisha kuwa uwajibikaji na utangamano
unaafikiwa nchini kwa kubainisha pale mpaka wa ‘usemi wa chuki’ unaanzia na kuishia.